Wadaiwa Sugu Kodi ya Pango kufikishwa Mahakamani.

Serikali inakusudia kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi na kuwafutia miliki zao kutokana na kukwamisha malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yatokanayo na kodi hizo.

Hayo yamebainishwa na waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka ujao wa fedha 2019/2020 ya kiasi cha shilingi bilioni 62.68.

Waziri Lukuvi amesema katika kipindi cha mwaka 2018/19 wizara ilipanga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 120 kutokana na kodi, ada na tozo mbalimbali za ardhi lakini hadi kufikia Mei 15 mwaka huu wizara ilikusanya bilioni 75.7 sawa na asilimia 63.1 ya lengo hali iliyosababishwa na uwepo wa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi.

Hapa waziri lukuvi akaainisha mikakati ya kuwezesha kukusanya kiasi cha bilioni 180 kutokana na tozo, ada na kodi zitokanazo na sekta ya ardhi kwa mwaka ujao 2019/2020 ikiwamo uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA katika kutunza kumbukumbu na kuhakikisha watu wote walio mijini wanarasimishiwa na kupatiwa hati na leseni za makazi.

Upande wa maoni ya kamati ya kudumu ya bunge ya ardhi, maliasili na utalii unaitaka wizara kuyaboresha mabaraza ya ardhi yaliyopo kwa kuyapatia vitendea kazi, huku baadhi ya wabunge wakitaka hatua kuchukuliwa dhidi ya wamiliki wa ardhi wasioyaendeleza maeneo yao ikiwamo kuwafutia leseni.

Comments

comments