Treni ya Majaribio Mradi wa SGR yazinduliwa.

Serikali imeanza mchakato wa ununuzi wa vichwa 22 vya treni, mabehewa 1,430 ya mizigo na Mabehewa 60 ya Abiria vitakavyotumika kwenye uendeshaji wa Reli ya kisasa ya SGR ambayo ujenzi wake unaendelea.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amefahamisha mpango huo wakati akizindua Safari ya kwanza ya majaribio ya Treni ya Wahandisi eneo la Soga lililopo Kibaha Mkoani Pwani, huku akiupongeza uongozi wa Shirika la Reli TRC kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.

Yapi Merkez inajenga Reli ya SGR awamu ya kwanza kutoka Dar Es Salaam hadi Morogoro ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 56 na awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora Mkoani Dodoma ujenzi wake umefikia asilimia 12 zote zikiwa na urefu wa kilomita zipatazo 722, ujenzi unaogharimu shilingi Trilioni 7.2 fedha za ndani.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania TRC Masanja Kadogosa amesema zoezi la majaribio ya awali ya treni ya wahandisi iliyotembea umbali wa kilomita 20 ni hatua muhimu ya kuhakikisha reli hiyo inapitika bila kikwazo kwani inakagua na kuimarisha miundombinu ya reli hiyo, kabla ya kuwasili treni rasmi.

Kukamilika kwa mradi huo utakaoongeza ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo, kutaiwezesha treni ya abiria kusafiri kwa umbali wa kilomita 160 kwa saa, na treni ya mizigo kusafiri kwa kilomita 120 kwa saa. Faida nyingine ni kuokoa muda wa safari, kuongeza usalama wa abiria na mizigo pamoja na kupunguza uharibifu wa barabara unaosababishwa na magari ya mizigo.

Comments

comments