Matumizi ya Nishati Mbadala Ukerewe,Wananchi kisiwa kutumia umeme wa jua

UMEME

Katika kuunga mkono jitihada za Rais Dk. John Pombe Magufuli za kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa viwanda, zaidi ya wakazi elfu thelathini wa visiwa kumi vya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, wanatarajia kunufaika na huduma ya Umeme Jua, utakaowawezesha kuanzisha viwanda vya uchakataji bidhaa mbalimbali.

Hii ni fursa ya kiuchumi katika Kisiwa cha Ghana, ambacho ni moja kati ya Visiwa kumi na tano vinavyokaliwa na watu wilayani Ukerewe , lakini changamoto kubwa inayovikabili Visiwa hivi ni ukosefu wa huduma za Nishati ya Umeme, hasa kutokana na ugumu wa ufikishaji wa miundombinu ya Nishati hiyo ndani ya Ziwa Victoria.

Francis Kibhisa ni mkurugenzi wa Kampuni ya Umeme Jua (Rex Energy), baada ya kubaini changamoto hizo anaingia makubaliano na Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe, kwa kusaini mkataba na wenyeviti wa vijiji vya Visiwa hivyo, ili kusambaza miundombinu ya Umeme Jua utakaowaondolea Wananchi adha ya kukaa gizani.

Akizungumzia matarajio yake Kibhisa, amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa kwa awamu ya kwanza utagharimu shilingi billioni 6.4 kati ya Billioni ishirini na moja, zitakazotumika katika miradi yote, utawahudumia zaidi ya wakazi elfu mbili na mia saba wa Kisiwa cha Ghana, katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

Baada ya kushuhudia makubaliano ya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo yaliyofanyika kati ya wenyeviti wa Vijiji na Kampuni ya Rex Energy, mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza Frank Bahati, anaeleza matumaini yake kutokana na mradi huo wa Nishati ya uhakika.

Comments

comments