Awamu ya Pili ya Mafunzo ya SADC kwa Wanahabari Yaanza.

Mafunzo Maalum ya umahiri kwa wanahari Waandamizi kwa ajili ya Mkutano wa Kilele wa jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika-SADC, yameendelea mjini Morogoro ikiwa ni awamu ya pili.

Jumla ya wanahabari 30 kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini wanashiriki mafunzo hayo ya umahiri ya siku tatu, ambayo yamelenga kuwapa uelewa zaidi wa kuandika Habari kuhusu SADC, ili kuwaongezea ufanisi kwenye kazi zao za kuhabarisha jamii wakati wa Mkutano wa kilele wa SADC utakaofanyika jijini Dar es salaam mwezi ujao.

Watoa mada katika Mafunzo hayo ni Dkt.Ayoub Rioba ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari la Utangazaji Tanzania-TBC, Balozi Hebert Mrango ambaye ni Mwakilishi wa Tanzania kwenye Makao Makuu ya SADC, Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mussa Uledi, na Dkt. Kaanaeli Kaale ambaye ni Mhadhiri wa Masuala ya Uandishi wa Habari.

Dkt.Rioba amewataka wanahabari hao kuijuza jamii ya Kitanzania ili iweze kufahamu umuhimu na maudhui ya SADC.

Mambo mengine ni nafasi ya Tanzania katika SADC, ambapo Bw. Mussa Uledi amebainisha kuwa mbali ya Tanzania kuwa Mstari wa mbele kaika Mapambano ya Ukombozi wa Bara la Afrika, imeshiriki pia katika kuundwa kwa asasi nyingi zilizo chini ya SADC na zinazosimamia masuala ya Uchumi, Siasa na Maendeleo ya jamii.

Aidha wanahabari wamehimizwa kuongeza ubunifu katika kuitangaza Tanzania kama mwenyeji wa mkutano wa kilele wa SADC mwaka huu na Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kuwa Mwenyekiti wa SADC jambo litakaloiongezea sifa Tanzania.

Comments

comments